Tuzungumze kuhusu kuharibika kwa mimba
Kupoteza mtoto wakati wa ujauzito kunaitwa kuharibika kwa mimba. Mmoja kati ya wanawake kumi huaribikiwa mimba katika maisha yake. Kama zilivyo maarufu, dhana potofu kuhusu kuharibika kwa mimba zinaweza kusababisha mwanamke na mpenzi wake wajihisi wapweke au wenye makosa. Kwa mfano, mazoezi, kujamiiana, au kunyanyua vitu vizito wakati wa ujauzito HAKUSABABISHI kuharibika kwa mimba.
Cha muhimu zaidi, kuharibika kwa mimba KAMWE sio kosa la mwanamke. Kiukweli, kuharibika kwa mimba kunaweza kutokea kutokana na sababu mbalimbali. Sababu ya mara kwa mara zaidi ni matatizo ya kinasaba ambayo humzuia mtoto kukua kwa kawaida. Hata hivyo, matatizo yanayohusiana na vinasaba kwa kawaida hutokea kwa bahati kadri mtoto anavyokua na ni nje ya uwezo wa mama kuyadhibiti. Kwa sababu hii, hakuna cha ziada sana unachoweza kufanya kuzuia kuharibika kwa mimba, lakini hivi hapa ni vitu UNAVYOWEZA kufanya kujilinda wewe mwenyewe na mtoto wako:
Fuata mahudhurio ya kliniki ya ujauzito inavyotakiwa
Epuka sababu za hatari zinazoweza kupelekea kuharibika kwa mimba kama uvutaji sigara, unywaji wa pombe, na matumizi ya madawa ya kulevya
Pata matibabu ya matatizo ya kiafya kama kisukari na shinikizo la juu la damu
Tumia vitamini wakati wa ujauzito
Asilimia 80 ya mimba zinazoharibika hutokea ndani ya miezi 3 ya mwanzo ya ujauzito. Kutokwa damu, tumbo kuuma, na maumivu chini ya kitovu ni dalili za mara kwa mara za kuharibika kwa mimba, lakini muda mwingine kunaweza kusiwe na dalili kabisa. Hivyo hakikisha unamjulisha daktari wako kuhusu dalili za ujauzito zisizo za kawaida moja kwa moja.
Dalili za kuharibika kwa mimba:
Kutokwa damu ukeni
Tumbo kuuma
Majimaji au nyama nyama kutoka ukeni
Kuwa na dalili hizi sio mara zote inamaanisha mimba yako inaharibika – ndio maana ni muhimu kuwasiliana na daktari wako kuona ikiwa unachopitia ni kitu cha kawaida.
Pia, sababu hizi zinazofuata zinaweza kuongeza uwezekano wa mimba yako kuharibika wakati wa ujauzito:
Kuwa na miaka zaidi ya 35
Kuharibikiwa mimba mara 2 au zaidi kipindi cha nyuma
Matatizo ya kizazi au mlango wa kizazi
Uvutaji sigara, unywaji wa pombe, na matumizi ya dawa za kulevya
Kuwa na uzito mdogo au uzito mkubwa
Kuharibikiwa mimba huleta changamoto za kihisia na kiakili. Hisia za kuomboleza na hali ya huzuni ni vitu vya kiasilia baada ya kuharibikiwa mimba. Hata hivyo, hauko peke yako. Ikiwa umeharibikiwa mimba, fikiria kushirikisha hisia zako na wanafamilia na marafiki zako wa karibu. Kutafuta makundi ya msaada ya wanawake wengine ambao pia wameharibikiwa mimba kunaweza kukutia moyo na kukupa kitulizo, pia. Mtaalamu wako wa afya anaweza pia kuwa na vyanzo vya nyongeza kwa ajili ya mbinu za kukubaliana na hali na machaguo ya matibabu. Kwa bahati nzuri, wanawake wengi ambao wameharibikiwa mimba huwa na mimba zenye afya baadae.
Je! Una maswali kuhusu kujamiiana, STIs, na uzazi wa mpango? Kumbuka unaweza kuchati na Nivi kwenye WhatsApp na Facebook Messenger muda wowote. Ni mazungumzo ya faragha, ya usiri, na ya bure!
Vyanzo